NYOTA WETU
Nyumba ya kifahari ya mwanamuziki mashuhuri wa Marekani, Sean Combs maarufu P. Diddy iliyoko Los Angeles imekuwa kivutio kikubwa wiki hii cha watu kufurika kuitazama na kupiga picha.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada kasri lake hilo kuvamiwa na mawakala wa Usalama wa Homeland Security Investigations (HSI) na kisha kupekuliwa, hali iliyoacha maswali mengi huku watalii wa ndani wakiingiwa na shauku ya kulitembelea.
Kwa mujibu wa kampuni kadhaa za mabasi ya kusafirisha watalii, kumekuwa na ongezeko kubwa la watu kutamani kufika na kuliona jumba hilo la kifahari tangu lilipopekuliwa na habari kusambaa kila kona kama moto wa kifuu.
Baadhi ya kampuni zimeripoti kuwa mabasi yao yameshajaa watu wanaotaka kwenda kwenye mjengo wa nguli huyo wa muziki wa hip-hop na R&B ambaye anakabiliwa na matatizo ya kisheria.
“Kumekuwa na watu wengi zaidi wakiuliza kuhusu nyumba ya Diddy wiki hii. Kwa hakika limekuwa jambo lenye shauku kubwa sana kwa wateja wetu,” amesema wakala mmoja wa kampuni ya kusafirisha watalii.
Ameongeza: “Sio kila siku unapata kushuhudia kitu kama hiki. Hakika inasisimua kuliko ziara zetu za kawaida.”
Mamlaka bado hazijaeleza kwa kina kuhusu sababu ya maofisa usalama kupekuwa nyumba za Diddy, hiyo ya Los Angeles na iliyoko Miami lakini vyombo vingi vya habari kama ABC na NBC News kupitia kwa maofisa ambao hawakutaka kutaja majina yao, vimedai kwamba Diddy anatuhumiwa kwa kuhusika na biashara ya ngono, unyanyasaji wa kijinsia na makosa yanayohusisha dawa za kulevya na silaha.
Diddy ambaye hajafunguliwa kesi rasmi, anakanusha madai hayo akidai kuna njama za kumbambikia kesi kwa sababu ambazo hazijui.
Mwaka 2001, Diddy alishitakiwa kwa kosa la kumiliki bunduki kinyume cha sheria pamoja na kutoa rushwa lakini alishinda kesi hiyo na ndipo akaamua kubadili jina lake la kimuziki kutoka Puff Daddy hadi P. Diddy.
Related Posts 📫
Discover more from JUNIITV.ONLINE
Subscribe to get the latest posts sent to your email.