HABARI KUU
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema linamshikilia mtuhumiwa aliyeonekana katika video ambayo ilisambaa katika mitaandao ya Kijamii na kupora vitu kwa mwananchi mmoja huko maeneo ya Burka kisongo Jijini Arusha.
Akitoa taarifa hiyo leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema Jeshi hilo lilipata taarifa kupitia mitandao ya kijamii iliyowaonesha vijana wawili wakiwa na pikipiki na kumpora mwanamke mmoja
Mara baada ya kupata taarifa hiyo mara moja walianza uchunguzi wa kina na kuwatambua wahusika wa tukio hilo ambapo Machi 28,2024 mtuhumiwa Jamal Idd Ramadhan (22) mkazi wa Ngusero alikamatwa ambapo Jitihada za kuwatafuta wengine zinaendelea.
SACP Masejo amesema Jeshi la Polisi Mkoani Arusha linaendelea kuwashukuru wananchi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu pamoja na waandishi wahabari kwa kufichua uhalifu katika Mkoa huo.