HABARI KUU
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kutekeleza mpango wa kulipumzisha Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma kuanzia Mei 15 hadi Agosti 15, 2024 ambapo shughuli za uvuvi zitazuiwa katika kipindi hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kalli, amewaambia wadau, viongozi na wavuvi wanaotumia ziwa hilo kuwa zoezi hilo ni sehemu ya kukuza sekta ya uvuvi nchini, kwa kuwa hatua hiyo itasaidia ongezeko la samaki na soko katika siku za usoni kutokana na uwepo wa samaki wa kutosha.
Kalli, amesisitiza juu ya umuhimu wa zoezi hilo katika Ziwa Tanganyika akisema ni kitovu cha mazao ya samaki kutokana na mazalia kuwa mengi na yenye kukidhi mahitaji ya watumiaji.
Ofisa Uvuvi Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ambakisye Simtoe amewataka wadau wa uvuvi kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha juu ya kupumzishwa kwa Ziwa Tanganyika ili kuchochea ongezeko la samaki katika ziwa hilo.