MICHEZO
Taarifa za uhakika ambazo zimetufikia zinasema kuwa mshambuliaji wa Azam FC aliyeaga klabuni hapo Prince Mpumelelo Dube ameamua kuwashitaki Azam FC kwa shirikisho la mpira nchini TFF.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa mshambuliaji huyo ameukana mkataba ambao Azam FC wanasema aliusaini na unaisha mwezi Juni 2026.
Mshambuliaji huyo ametinga TFF na mkataba ambao anasema ni halali ambao unafikia ukomo wake mwisho mwa msimu huu yaani Juni 2024 na kuukana ule ambao Azam wanasema alisaini wa muda mrefu.
Mshambuliaji huyo amepeleka mkataba alionao na ambao anautambua yeye, nyaraka mbalimbali pamoja na vielelezo vingine kuthibishisha kuwa mkataba wake halali anaoutambua ni alionao unaotamatika mwishoni mwa msimu huu.
Hivi karibuni mchezaji huyo aliwaaga Azam kupitia akaunti yake ya Instagram huku akiwashukuru watu mbalimbali katika klabu hiyo kama viongozi wa timu, idara mbalimbali pamoja na mashabiki wa klabu hiyo.
Klabu ya Azam ilijibu mapigo Kwa kusema mshambuliaji huyo bado ni mchezaji wao kwani anao mkataba mrefu na wauza ice cream hao mpaka 2026.
Klabu hiyo imeenda mbali na kumwambia mchezaji huyo kuwa kama anataka kuondoka afuate utaratibu wa kuvunja mkataba na sio kuaga akiwa bado ni mali yao.
Kwa kujibu wa klabu hiyo ni kwamba thamani ya kuvunja mkataba wa mchezaji huyo ni 700m hivyo afike mezani na atimize matakwa ya kifungu hicho ili wamuachie huru.
Taarifa ambazo tunazo ni kuwa Azam FC imekuwa ikimuandikia barua mshambuliaji huyo kila baada ya siku tatu ikimhitaji aripoti kazini kuendelea na majukumu yake.