MICHEZO
Kocha Mkuu wa Newcastle United, Eddie Howe amesema klabu hiyo haina nia ya kusikiliza ofa ya kumuuza Mshambuliaji wake, Alexander lsak katika dirisha kubwa msimu ujao.
Mshambuliaji huyo raia wa Sweden, alitua Newcastle United mwaka juzi kwa pauni milioni 63 na kuonyesha makali katika michuano mbalimbali.
Pamoja na kukosa baadhi ya michezo kutokana na majeraha, lakini Isak amefunga mabao 14 na kutoa pasi moja ya bao katika michezo 21 ya Ligi Kuu ya England msimu huu.
Kutokana na ubora wake hasa katika kufumania nyavu, klabu mbalimbali za England zimekuwa zikiiwania saini ya Mshambuliaji huyo wa zamani wa Real Sociedad ya Hispania.
Isak ambaye ameripotiwa kuivutia klabu ya Arsenal huku yeye mwenyewe akiwa tayari kutimka Newcastle kama itamruhusu, lakini kocha wa kikosi hicho Howe amesema hawana mpango wa kumuuza nyota huyo.
“Ana kipaji cha hali ya juu na hakuna mtu ambaye anahusiana na Newcastle angetaka kumpoteza,” alisema.
Wakati huu ambao Callum Wilson anauguza majeraha, Howe anamtegemea Isak kama Mshambuliaji pekee hatari anayeweza kumpa mabao ya kutosha katika kikosi hicho.
Msimu uliopita, Isak mwenye umri wa miaka 24, alifunga mabao 10 na kutoa pasi moja ya bao katika mechi 22 za Ligi Kuu ya England.