HABARI KUU
Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba, Amour Hamad Salehe, amekanusha taarifa za uzushi zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa sadaka ya Shilingi 5,000 akisema taarifa hizo ni upotoshaji.
RC Amour ameyasema hayo kufuatia taarifa za baadhi ya watu kuandika katika mitandao ya kijamii kuhusu zoezi hilo, akisema yupo Mfanyabiashara ambaye ana utamaduni wa kufanya zoezi hilo na si vyema kuhusisha taarifa zenye taharuki kwa jamii.
Amesema, “kuna Mfanyabiashara mmoja amekuwa na utamaduni zaidi ya miaka sita wa kutoa sadaka kwa watoto mayatima kila ifikapo mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kwa awamu ya kwanza zoezi la utoaji sadaka lilifanyika kwa ufanisi mkubwa.”
“Awamu ya pili Wananchi walipeana taarifa iliyohamasisha wananchi kufika kwa wingi. Waliokuwapo kwenye mpango walipata sadaka kama ilivyopangwa. Kwa ubinadamu wake wote waliokuwa nje ya mpango walipewa kila mmoja Sh 5,000 kama nauli ya kurejea nyumbani na sio sadaka,” alifafanua RC Amour.
Aidha, katika hatua nyingine Mfanyabiashara huyo anayejulikana kwa jina la Abas Haji anayemiliki Hotel kwenye eneo la Mgogoni Pemba, alisema, “msaada huu sio kutoka kwa Mama Samia wala Ikulu au watu wengine. Msaada huu ni mimi kama mimi na familia yangu.”