MICHEZO
Kocha Mkuu wa Liverpool Jurgen Klopp ameionya Manchester United akisema watachezea kichapo kutoka kwa Arsenal mwezi ujao ikiwa watacheza kama walivyocheza dhidi ya kikosi chake.
Klopp alitaka Liverpool kutulia baada ya timu hiyo kutoka sare ya kufungana mabao 2-2 katika mchezo wa Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Old Trafford Jumapili (Aprili 07).
Man United bado inaweza kusaidia kikosi cha Klopp wakati watakapokuwa wenyeji wa Arsenal, vinara wapya, baada ya mechi za wikiendi iliyopita.
Hata hivyo, Klopp anahofia Man United kwani wanahitaji kuwa ngangari zaidi na kuongeza kiwango chao ikiwa kama wanataka kusimamisha kikosi cha kocha Mikel Arteta.
Alipoulizwa kama ataishangilia United Mei 11, mwaka huu, alisema: “Ikiwa bado tupo katika mbio za ubingwa, itakuwa nzuri”.
“Lakini Arsenal ni timu nzuri yenye kucheza kandanda safi, lakini ikiwa (United) itacheza kama walivyocheza na sisi, Arsenal itashinda mchezo huo, nina uhakika kwa asilimia 100, lakini samahani kwa hilo.”
Mchezo huo wa juzi ni wa pili kwa Liverpool kwenye Uwanja wa Old Trafford ndani ya wiki tatu na walipiga jumla ya mashuti 53 katika mechi hizo mbili lakini hawakushinda hata moja.
Walifungwa mabao 4-3 katika Robo Fainali ya Kombe la FA Machi 17, mwaka huu na sasa wamepoteza pointi mbili za Ligi Kuu katika mbio zao za kusaka ubingwa, huku wakipambana na Arsenal na Manchester City.
“Ni kweli tungeshinda mechi zote lakini hatukuweza,” alisema Klopp.
Hata hivyo, alisema mashabiki wa Liverpool hawatakiwi kukata tamaa kuhusu uwezo wa klabu yao katika msimu wa mwisho wa kocha huyo Mjerumani.