HABARI KUU
Polisi nchini Brazil wanamshikilia Érika de Souza Vieira kwa tuhuma za kupeleka maiti ya mjomba wake Paulo Roberto Braga (68) benki , ili achukue mkopo kwa jina lake ambao ni Dola 3,250 za Kimarekani sawa shilingi Milioni nane.
Muda mfupi baada ya Érika kuingia katika moja ya benki huko
Rio de Janeiro akiwa na mwili huo wa mjomba wake alikamatwa na ameshtakiwa kwa kosa la kukiuka sheria inayolinda maiti na kujaribu kuiba na kujipatia pesa kwa njia ya ulaghai.
Picha ya video iliyopandishwa na kituo cha televisheni cha Aljazeera inamuonesha mwanamke huyo akimshikisha kalamu marehemu huyo na kumsihi aweke saini kwenye karatasi ya benki huku pia akiwa ameshikilia kichwa chake.
Maofisa wa benki walishtuka baada ya kuona mwili wa ‘mteja’ huyo ukiwa umepauka sana na ndipo waliposema hayupo sawa.
Polisi nchini Brazil wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kufahamu pia kama kuna watu wengine wanaohusika.