NYOTA WETU
Imefahamika kuwa uongozi wa klabu ya Chelsea unajipanga kumsainisha mkataba mpya kiungo mshambuliaji Cole Palmer, baada ya kuonesha umahiri mkubwa kwenye kikosi cha klabu hiyo msimu huu 2023/24.
Nyota huyo, ambaye alisajiliwa kutoka Manchester City majira ya joto yaliyopita, amefunga mabao 25 katika michezo 42 kwenye michuano yote katika msimu ambao umekuwa mbaya kwa The Blues.
Taarifa zilizochapishwa kwenye Gazeti la The Sun zinaeleza kuwa Chelsea inapanga kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Cole Palmer kuhusu kandarasi mpya kabla ya mwisho wa msimu huu, huku nyota huyo akiwa na uwezo wa kucheza Fainali za Mataifa ya Bara la Ulaya ‘Euro 2024’.
Mkataba wa sasa wa Cole Palmer unatarajiwa kumalizika 2030, wakati Chelsea hawana haraka ya kukamilisha makubaliano, wanakusudia kumzawadia Palmer kwa kiwango kikubwa na nyongeza ya mshahara.
Nyota huyo wa zamani wa Manchester City kwa sasa analipwa zaidi ya Pauni 80,000 kwa juma ambayo ni chini ya wachezaji wenzake wengi wa Chelsea, ambao wengi wao wameshindwa kuonesha uwezo chini ya Pochettino msimu huu 2023/24.
Mshambuliaji Raheem Sterling, anadaiwa kulipwa takriban Pauni 325,000 kwa juma na Uongozi wa Chelsea unanuia kupunguza wigo kati ya Palmer na wachezaji wanaolipwa fedha nyingi katika klabu hiyo huku wakiendelea kujitengenezea siku zijazo.