MICHEZO
Mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup) kati ya USM Alger ya Algeria na RS Berkane ya Morocco haujafanyika baada ya wageni RS Berkane kuzikataa jezi walizozikuta kwenye Vyumba vya Uwanjani wakidai sio zao.
Awali, RS Berkane walidai jezi zao zilizuiwa Uwanja wa Ndege walipowasili Algeria, wakawaambia hawataruhusiwa kuzitumia kwa kuwa zina Bendera ya Morocco, jambo ambalo lilipingwa na RS Berkane, wakasisitiza wanataka kuzitumia jezi hizo la sivyo hawataingia uwanjani kucheza.
Imeelezwa kuwa Msafara wa RS Berkane ulipofika vyumbani ukakuta jezi ambazo hazina bendera ya Morocco na hivyo wakagoma kuingia uwanjani, baada ya majadiliano marefu wameondoka uwanjani.
Wadau wanasubiri maamuzi kutoka kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kuwa Kidiplomasia Algeria na Morocco hazina Uhusiano mzuri na hiyo inatajwa kuwa chanzo cha Algeria kukataa uwepo wa Bendera ya Morocco kwenye jezi.