HABARI KUU
Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara ameitaka Serikali kupeleka umeme kwa Wachimbaji wadogo Msege akidai shughuli hiyo ilisimama mara baada ya Waziri kuahirisha ziara ya kutembelea eneo hilo.
Waitara ameyasema hayo hii leo Aprili 23, 2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiuliza swali kwa Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, kutaka kujua ni lini Serikali itapeleka umeme kwa Wachimbaji hao.
Amesema “Naibu Waziri wa Nishati alipanga ziara jimbo la Tarime Vijijini kwenye kata ya Nyarokoba kwa Wachimbaji wadogo Msege, ambapo wakati wa ziara hiyo walileta nguzo na kazi ilenda kwa kasi sana, ila alipo hairisha ziara, kila kitu kilisimama.”
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nishati, Judithi Kapinga ametoa maelekezo kwa Meneja wa Mkoa wa Mara kwa sehemu zote ambazo zimepelekwa nguzo shughuli ziendelee na maeneo ya Wananchi yapate umeme kwa wakati.
“Haiwezekani shughuli zisimame kisa ziara ya kusitishwa, nimuelekeze katika maeneo yote yaliyopelekwa nguzo shughuli zifanyike kwa haraka iwezekanavyo na maeneo yale Wananchi wapate umeme kwa wakati,” alisema Naibu Waziri Kapinga.