MICHEZO
Klabu ya USM Alger ya Algeria itatozwa faini ya USD $50,000 zaidi ya milioni 129 kwa kutojitokeza kwenye mchezo wa jana Aprili 28, 2024 dhidi ya RS Berkane ya Morocco, mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika uliopaswa kupigwa kuanzia majira ya saa 4:00 usiku kwa saa Afrika Mashariki.
Klabu hiyo pia itatakiwa kuwatalipa RS Berkane USD $15,000 zaidi ya milioni 38 kama fidia ya kulipia gharama za mechi ya kwanza ambayo Berkane walisafiri hadi Algeria na mchezo haukufanikiwa kuchezwa kwa sababu za kisiasa.
Aidha upo uwezekano wa klabu hiyo kutolewa kwenye mashindano yoyote yaliyochini ya Shirikisho la Mpira Afrika (CAF).
Katika mchezo wa jana, USMA walionekana wakitoka katika hoteli waliyofikia huko Morocco tayari kwa kuelekea uwanjani kwaajili ya mchezo huo lakini muda wa mchezo ulipofika hawakutokea ndani ya uwanja.
Awali CAF iliipa ushindi wa mabao 3-0 RS Berkane dhidi ya USMA Alger katika mchezo wa kwanza uliopaswa kuchezwa Aprili 21, 2024 baada ya kushindikana kupigwa kutokana Mamlaka za soka Algeria na serikali kuzuia jezi za Berkane zenye ramani ya Morocco wakisisitiza kuwa hawaitambui ramani ya Morocco iliyopo kwenye jezi za Berkane kwa sababu inajumuisha eneo la Sahara Magharibi na wanaamini kwamba Morocco kudhibiti eneo hilo ni haram.