MICHEZO
Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limemtangaza Mwamuzi kutoka Mauritania Beida Dahane kusimamia Teknolojia ya Video ya Usaidizi kwa Mwamuzi wa Kati ‘VAR’ katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali Ligi ya Mabingwa Barani humo, baina ya Esperance na Al Ahly itakayochezwa Tunis, Tunisia, Mei 18.
Jina la Dahane limekuwa maarufu nchini Tanzania baada ya kuchezesha mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali kati ya Mabingwa wa Soka Afrika Kusini Mamelodi Sundowns dhidi ya Mabingwa wa Tanzania Bara Young Africans uliochezwa Pretoria, Afrika Kusini, Aprili 5.
Katika mchezo huo, Dahane alitoa uamuzi uliozua mjadala baada ya kutoamuru mpira uliopigwa na Stephane Aziz Ki kuwa bao licha ya kuonekana ulivuka mstari na kuingia golini.
Katika mchezo huo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Mwamuzi wa kati atakuwa ni Mustapha Ghobal kutoka Algeria.
Katika uteuzi huo wa CAF, mchezo wa Mkondo wa Pili ambao umepangwa kuchezwa jijini Cairo, Misri Mei 25, Mwamuzi wa Kati atakuwa Jean Jacques Ndala kutoka DR Congo.
Mwamuzi ambaye atasimamia VAR katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Fainali atakuwa Benbrahim Lahlou kutoka Algeria.
Ikumbukwe kuwa Dahane ni miongoni mwa Waamuzi 12 wa Afrika ambao watachezesha Michezo ya Olimpiki itakayofanyika nchini Ufaransa kuanzia Julai 26 hadi Agosti 11.
Related Posts 📫
Discover more from JUNIITV.ONLINE
Subscribe to get the latest posts sent to your email.