MICHEZO
Mabingwa wa Soka Tanzania bara Young Africans ni kama wameamua kujiimarisha zaidi kwa ajili ya msimu ujao, inaelezwa chini ya Rais wa klabu hiyo, Hersi Said, wameanza mazungumzo na nyota wa Simba SC Kibu Denis.
Mkataba wa mchezaji huyo na Simba SC unaisha mwishoni mwa msimu huu ingawa Simba SC wanataka kumbakisha mchezaji huyo, taarifa zinasema tayari uongozi wa Young Africans umeingilia kati na kuanza mazungumzo ya kumsajili nyota huyo.
Inaelezwa Young Africans wameweka mezani ofa ya shilingi milioni 150 pamoja gari kwa mchezaji huyo wa zamani wa Mbeya City na tayari uongozi wa Young Africans upo kwenye mazungumzo na wawakilishi wa mchezaji huyo, ambaye mkataba wake unafika ukingoni mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Taarifa zilizopatikana jijini Dar es salaam zinasema viongozi wa Young Africans wameanza mazungumzo na nyota huyo na kuweka ofa hiyo mezani lakini Kibu hajatoa tamko lolote la kukubali au kukataa ofa hiyo iliyokwa mezani na mabosi wa Young Africans.
Mtoa taarifa amesema Kibu ameingia katika orodha ya wachezaji wanaotakiwa na Young Africans baada ya Kocha Miguel Gamondi kutaka kuongezewa mshambuliaji mzawa kwa lengo la kuimarisha safu hiyo ya ushambuliaji.
“Licha ya kuwekewa ofa hiyo hadi sasa Kibu hajasema lolote kuhusu kukubali au kukataa, hii inatokana na kusubiria waajiriwa wake Simba SC kuhusu ofa yao, pia Azam FC nao wameonyesha nia ya kuhitaji huduma ya nyota huyo,” amesema mtoa taarifa hizo.
Amesema Simba SC nao hawajakata tamaa ya kumbakisha nchezaji huyo kwani nao wamemwekea ofa mezani.
“Sasa hivi Kibu ndio mwenye uamuzi kuamua wapi atie saini, ana ofa mbili za uhakika lakini pia Azam FC wameonyesha nia ya kumtaka pia,” amesema mtoa habari huyo.