HABARI KUU
Watu saba wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa kufuatia ajali iliyohusisha gari aina ya Toyota Noah, yenye namba za usajili T101 DKB kugongana uso kwa uso na Lori aina ya Man lenye namba za usajili RL 1801 katika barabara kuu ya Dodoma – Morogoro.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema ajali hiyo imetokea hii leo eo Mei 14, 2024 majira ya saa 8.00 asubuhi, katika eneo la Dakawa lililopo Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro, ambapo gari hiyo aina ya Noah ilikuwa ikielekea Morogoro, huku Lori likielekea Dodoma.
Amesema, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa Dereva wa Lori ambaye alishindwa kulimudu gari na hivyo kwenda kuligonga gari hilo dogo lililokuwa limebeba abiria.
Kamanda Mkama amesema hata hivyo bado wanaendelea kumtafuta Dereva wa Lori ambaye alisababisha ajali, ambaye alikimbia baada ya tukio.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mvomero, Francis Paul Mogera amethibitisha kupokea miili hiyo pamoja na majeruhi huku, akisema majeruhi wanaendelea kupokea matibabu kwani wana majeraha madogo na mshtuko wa kawaida.
Mmoja wa majeruhi katika ajali hiyo, Maimuna Ally Salum amesema wakiwa safarini dereva wa gari la mizigo alitaka kulipita gari jingine kwa karibu ndipo gari zikakutana uso kwa uso.
“Tumetoka Dumila asubui tulipanda Noah kufika maeneo ya bwawa la taka mbele kidgo gari la mizigo ilikuwa inatokea Dar es salaam ile gari ya mizigo ikawa inataka kuovertake na sisi tupo karibu ndo akaja akatupush uso kwa uso,” alisema Maimuna.