MICHEZO
Ushindi wa mabao 2-0 walioupata Manchester City dhidi ya Tottenham Hotspur katika uwanja wa ugenini umewafanya wajiweke katika mazingira mazuri zaidi ya kulitwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (English Premier League).
Mabao ya Manchester City katika pambano hilo gumu la yamefungwa na mshambuliaji wake kinara wa ufungaji mabao Erling Haaland katika kipindi cha pili cha mchezo huo.
Ushindi huo umevunja matumaini ya Arsenal kukitwaa kikombe hicho ambacho mara ya mwisho walikitwaa Mwaka 2004.
Ushindi huo wa Manchester City umewafanya wafikishe pointi 86 na kushika usukani wa ligi hiyo na kuwaacha Arsenal wakiwa nafasi ya pili na pointi zao 86, huku timu hizo zikiwa na michezo 37 kila mmoja.
Michezo ya mwisho ya timu hizo ndiyo itakayoamua bingwa atakuwa nani. Arsenal watakuwa nyumbani kwao Emirates Stadium kucheza dhidi ya Everton, huku City nao watakuwa nyumbani kwao Etihad Stadium kucheza dhidi ya West Ham.
Kama City watafanikiwa kushinda kikombe hicho watakuwa wameshinda mara nne mfululizo wakiwa chini ya kocha wao Pep Guardiola.