HABARI KUU
Rais wa Kenya, William Ruto na mgeni wake Rais wa Uganda, Yoweri Museveni wametia saini mikataba mbalimbali ya ushirikiano, ikiwemo usafirishaji wa mafuta ya Petroli kutoka Kampala kupitia Bandari ya Kenya.
Utiaji wa saini huo, hautaathiri mpango wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka mjini Eldoret katika mkoa wa bonde la ufa nchini, Kenya hadi Uganda.
Ziara hiyo inafuatia kikao cha pili cha Tume ya Pamoja ya Mawaziri (JMC) kilichomalizika hivi karibuni kati ya Kenya na Uganda, ambapo mikataba saba ya makubaliano (MoU), ilisainiwa ikiwemo utumishi wa umma, elimu, maendeleo ya biashara ndogo ndogo, michezo, masuala ya vijana, biashara na uwekezaji.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Kenya, Musalia Mudavadi amesema ziara ya rais Museveni ni muhimu ikilenga kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.