HABARI KUU
Wakati serikali ikipiga marufuku biashara holela ya uuzaji wa dawa na matumizi ya vifaa tiba kinyume Cha utaratibu Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba nchini (TMDA) kanda ya magharibi imefanya msako maalum wilayani Kahama mkoani Shinyanga na kufanikiwa kumkamata Mkazi wa Mtaa wa Mwime, Charles Ngasa akiuza dawa kwenye duka lake kinyume na sheria.
Operesheni hiyo maalumu imefanyika May 16, 2024 ikiongozwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba nchini (TMDA) katika wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga.
Venancy Burushi ni Mkaguzi kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba nchini (TMDA) kanda ya ziwa magharibi ameeleza namna walivyoendesha msako huo hadi kubaini uwepo wa dawa ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Akizungumza wakati wa msako huo Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwime Dogo Mhenziwa amekiri kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya uzwaji wa dawa zilizokwisha muda wa matumizi kwenye duka hilo huku baadhi ya wakazi wakiiomba serikali kuchukua hatua ya kudhibiti uuzaji wa dawa hizo.
Akizungumza wakati wa operesheni hiyo Mmiliki wa duka hilo la uuzaji wa dawa za binadamu Charles Ngasa ameomba radhi kwa kukutwa na dawa hizo.
“Naomba chini ya miguu kwa picha iliyojionyesha kwa jinsi nilivyopata dawa hizi sina jinsi ya kujitetea”, amesema Charles Ngasa.
Kwa upande wake Dk. Edgar Mahundi Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Magharibi ametaja athari za dawa zilizokwisha muda wa matumizi ikiwemo kifo kwa mtumiaji.
“Madhara ya dawa zilizokwisha muda wa matumizi ni makubwa kwanza zinasababisha vimerea sugu vya magonjwa, baadhi ya viongo vya mwili kutofanya kazi lakini pia inaweza kupelekea kifo”, amesema Dk Edgar Mahundi.