HABARI KUU
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limetangaza kuzuia jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais Felix Tshisekedi huko Kinshasa.
Hayo yamebainishwa na Msemaji wa jeshi la DR Congo Brig Jenerali Sylavin Ekenge katika kituo cha runinga cha taifa RTNC TV ambapo amesema kuwa washukiwa kadhaa wamezuiliwa na “hali sasa imedhibitiwa”.
Tangazo hilo linajiri saa chache baada ya watu wenye silaha kushambulia nyumba ya Vital Kamerhe ambaye ni mkuu wa zamani wa majeshi na mshirika wa karibu wa Rais Felix Tshisekedi.
Mashuhuda wa tukio hilo wanasema kundi la watu takriban 20 wakiwa wamevalia sare za jeshi walishambulia makazi hayo na ufyatulianaji wa risasi ukafuatia.
Rais Tshisekedi hajatoa tamko lolote kuhusu tukio hilo.
Wakati huo Balozi wa Japani katika mji mkuu wa Congo amewaonya wajapani walioko DRC kutotoka nje.