HABARI KUU
Mkazi wa Manispaa ya Bukoba Mzee Pius Ngeze (70), amesema anahofia balaa kubwa kutokea katika Mkoa huo kumezwa na ziwa Victoria, kutokana na kukosekana kwa mikakati mahsusi wala uchunguzi, ili kubaini kwanini Tetemeko, Mafuriko na majanga mengine yanatokea mara kwa mara na kusababisha athari kwenye jamii.
Ngeze ambaye pia ni mmoja wa Wazee washauri wa Mkoa huo, amesema hata mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia Ijumaa ya Mei 10, 2024 ilisababisha Mafuriko katika maeneo mbalimbali, lakini hakuna tamko la watafiti la kuipanga jamii katika makazi rasmi, ili kukwepa maafa zaidi ya kupewa tahadhari pekee.
Amesema, “ndani ya Mkoa Kagera Manispaa ya Bukoba mafuriko yamesababisha adha kwa wakazi nikiwemo mimi kwani vitabu ninavyozalisha na mali zilizokuwa ndani ya nyumba zenye thamani ya milioni 100, zimeharibika na kukosa sifa zikiwemo nyaraka na vitabu. Nani atatuambia kuhusu hili mana hali imezidi kuwa mbaya Kagera kila siku matukio.”
Mzee Ngeze ameongeza kuwa, Serikali inatakiwa kutoka na sera, ili kuwashirikisha Wananchi katika ujenzi wa makazi yatakayostahimili matetemeko na kukwepa mabonde kuepuka maafa, kwani Bukoba kila mwaka hupita matetemeko madogo madogo yasiyopungua 20, vimbunga vya majini hadi nchi kavu hali ambayo haijawahi kutokea.
“Ninahoji kama mwananchi wa kawaida, hii hali ya Ziwa kujaa kiangazi na matetemeko kuja kila baada ya miezi miwili vina uhusiano gani? sikupata jibu la kuridhisha lakini niliwahi kumuambia Mkuu wa Mkoa na RAS wakahi huo jambo hili lakini kama hawatafanyia kazi hili hali inazidi kutisha.
Dhoruba wakati wa msimu wa mvua si jambo geni lakini kwa mwaka huu, mvua kubwa zimeshuhudiwa kutokana na mfumo wa hali ya hewa wa El-nino, huku Wataalamu wakisema mabadiliko ya tabianchi pia yamechochea hali hiyo ambayo imeleta madhara maeneo mengi.