HABARI KUU
Kiongozi wa ngazi ya juu nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amemteua Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Muhammad Mukhbar kuwa rais kufuatia kifo cha Ibrahim Raisi katika ajali ya Helikopta hapo jana Mei 19, 2024.
Kwa mujibu wa katiba ya Iran, makamu wa kwanza wa rais atachukua wadhifa huo iwapo rais atafariki, kuondolewa madarakani, kujiuzulu au kuwa mgonjwa kwa kipindi cha zaidi ya miezi miwili.
Raisi, ambaye alifariki katika ajali hiyo pamoja na Waziri wake wa Mambo ya Kigeni Hossein Amir-Abdollahian na maofisa wengine saba wa Serikali, alikuwa anakaribia mwisho wa muhula wake wa kwanza wa kipindi cha miaka minne kama rais.
Ayatollah Ali Khamenei ndiye kiongozi aliye na mamlaka makubwa kuhusiana na masuala yoyote ya kitaifa na hata hivyo uchaguzi mkuu wa Taifa hilo unatarajiwa kufanyika katika kipindi cha siku 50 kumchagua rais kikatiba ambapo Spika wa Bunge, Rais wa Mahakama na Makamu wa Rais, wamepewa jukumu la kuandaa uchaguzi huo.
Mukhbar (68), aliyezaliwa mji wa Dezful, Kusini Magharibi mwa jimbo la Khuzestan na aliyehudumu nafasi tofauti za Serikali, aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais Raisi alipochukua wadhifa huo mwezi Agosti mwaka wa 2021 na Iran hupiga kura kumchagua rais mpya kila baada ya miaka minne tangu taifa hilo la Kiislamu kufanya uchaguzi wake wa kwanza mwaka wa 1980.