MICHEZO
Kocha Mkuu wa Chelsea Mauricio Pochettino amefichua alikuwa na mazungumzo wakati wa chakula cha jioni na Mmiliki mwenza wa Klabu hiyo Todd Boehly Mmiliki jijini London.
Pochettino amefichua hilo katika kipindi hiki ambacho mashabiki wengi wa Chelsea wanaamini kikosi chao kinahitaji kufanyiwa maboresho kwa kuongezewa baadhi ya wachezaji ili kiwe na ubora wa kushindani kwa msimu ujao wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa.
Pochettino amesema: “Sijui kama hilo la usajili litatokea au la. Sina wazo lolote kuhusu hili. Ninachoweza kukwambia ni usiku wa kuamkia jana, Todd alinialika kwa chakula cha jioni na mkutano wetu ulikuwa mzuri sana. Tulipata chakula kwa furaha na mazungumzo yetu yalikwenda vizuri sana.
“Inatosha kufahamu kuwa nilikuwa na kiongozi wangu kwa mazungumzo na chakula cha jioni. Sitazungumza kwa undani zaidi juu ya hili. Lakini ikiwa nitakualika wewe na tukala chakula cha jioni, sio kwa mambo mabaya. Ninaamini umenielewa ninamaanisha nini hapo.
“Siku zote, unaweza kuimarika. Ninaamini kikosi changu kitakuwa bora zaidi msimu ujao kwa sababu watakuwa na uzoefu baada ya kuwa pamoja kwa msimu mmoja.
“Hiyo ndiyo faida ya kuwa imara na thabiti na kutofanya mabadiliko mengi. Msimu ujao tukiendelea 80-85% ya kikosi, kwa hakika, ni hatua kubwa mbele kwa sababu ni mwendelezo wa mawazo na maarifa kati yao. Hilo ni muhimu kwa klabu.