HABARI KUU
Profesa Rwekaza Mukandala amesema kuzama kwa Mv. Bukoba kulitokana na sababu kadhaa, kubwa ikiwa ni meli kukosa ustahimilivu na kulala upande mmoja na kisha kuzama.
Profesa Mukandala amesema hayo leo katika mhadhara wa uprofesa uliyofanyika katika Ukumbi wa Nkurumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye mafunzo ya kutoka katika kujifungua kwa uchungu wa kushinikiza, maisha ya mateso, na kifo cha maumivu cha MV. Bukoba.
Amesema sababu zingine ilikuwa ni uchache wa maji kwenye baadhi ya matenki, wingi wa abiria zaidi ya kiwango ambacho meli ilipaswa kubeba, na wingi wa mizigo.
Sababu nyingine amesema ilikuwa uzembe wa wafanyakazi wa meli na taasisi husika kushindwa kusimamia vizuri uendeshaji wa meli.
Aidha Profesa Mukandala amesema kuwa meli ya MV. Bukoba haikuwa na hali nzuri ya kusafiri kwani ilionesha dalili za kukosa ustahimilivu mapema.