HABARI KUU
Duru za ndani nchini Israel zinasema serikali ya taifa hilo itatoa karipio kali kwa mabalozi wa Ireland, Norway na Uhispania kutokana na mpango wa serikali zao wa kulitambua taifa la Palestina juma lijalo.
Taarifa hiyo inatolewa wakati ndani ya Ukanda wa Gaza Wapalestina 35 wakiripotiwa kuuwawa kwa mashambulizi ya jeshi lake usiku wa kuamkia leo.
Mabalozi hao wameitwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, ambapo pamoja na masuala mengine wataoneshwa vidio ambazo hazijaoneshwa hadharani za Hamas wakiwachukua mateka wanawake wakati wa shambulio la Oktoba 7 kwa Israeli ambalo lilizusha vita vya Gaza.
Israel pia imewaita tena mabalozi wake huko Dublin, Oslo na Madrid kwa mashauriano.
Akizungumzia suala la utambuzi wa taifa la Palestina Waziri wa Mambo ya Nje wa Colombia, Luis Gilberto Murillo amesema wanaamini na wana uhakika kwamba nchi nyingi zaidi zitaitambua Palestina ingawaje Umoja wa Mataifa uliridhia, katika muktadha wa Makubaliano ya Oslo, kwamba suluhisho la serikali mbili linapaswa kuundwa.