HABARI KUU
Watu 11 wakiwemo raia watatu kigeni wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa, baada ya mfumo wa joto wa kiwanda cha kuzalisha sukari cha Mtibwa kilichopo Turiani Mkoani Morogoro kulipuka wakati wakijiandaa kuanza uzalishaji.
Akizungumza na Dar24 Media, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shaban Marugujo amesema mlipuko huo ulitokea majira saa 7 usiku wa kuamkia hii leo Mei 23, 2024.
“Ni kweli watu 11 wamefariki dunia na wawili kujeruhiwa baada ya mripuko wa mpira wa joto wakati wanajiandaa na uzalishaji wa sukari pale kiwandani Mtibwa,” alisema Kamanda Marugujo.
Watatu kati ya waliofariki katika tukio hilo ni raia wa kigeni kutoka nchini Kenya, Brazil na India, huku miili ya Marehemu hao ikihifadhiwa katika hospitali ya Mtibwa Sugar na majeruhi wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Misheni Bwagala huku waliofariki wakiwa ni wataalamu wa umeme, waliokuwa katika chumba cha kuendesha mitambo hiyo.
“Katika uzalishaji wa Sukari kuna kiwango cha joto ambacho kinatakiwa kifikie, badala yake wakati wa watu hao wakiwa kwenye maandalizi ya uzalishaji walikuwa wakisubiri kile kiwango cha joto ndipo ukatokea mlipuko huo na kuwakuta watu 11 ambao kwa kiwango kile cha joto wakafariki papo hapo,” alifafanua Marugujo..
Aidha, amesema “Chanzo halisi cha mlipuko huo bado hakijapatikana na bado tunaendelea na uchunguzi, timu nzima ipo hapa kiwandani tangu usiku huo na mpaka sasa tunaendelea na tukikamilisha tutatoa taarifa rasmi kuhusu tukio hili.”