Paul Okoye, maarufu kama Rudeboy kutoka kundi la muziki wa Afrobeats la PSquare amezua gumzo mitandaoni baada ya kuwashauri wanaume pia kukumbatia hulka ya kukataa mpenzi wa kike asiye na hela, kama wanavyofanya wanawake wengi.
Ifahamike kwamba idadi kubwa ya wanawake wakati wa kufanya chaguo la mwanamume wa kuingia katika uchumba naye, wengi huangalia kigezo cha ‘mwanamume mwenye hela’ na kama huna hela mtoto wa kiume unakataliwa papo hapo.
Sasa Rudeboy anahisi kwamba ni wakati wanaume pia waanze kufuata mkondo huo, akisema kuwa kama wanawake wanavyochagua mwanamume mwenye hela wakati wao hawana chochote cha kuchangia katika mapenzi, basi pia wanaume waanze kuchagua ‘mwanamke mwenye hela’ na kama hana akwende zake pia.
Msanii huyo kupitia instastory yake aliwauliza wanawake watajihisi vipi ikiwa wanaume pia wataanza kuchagua wanawake wenye hela, je wengi wao watapata wapenzi kweli ama wataishia pia kulia.
Rudeboy alisema kwamba wanaume wengi wanapitia aibu zilizokithiri mikononi mwa wanawake wanapopeleka ombi lao la kutaka mapenzi, wengi huishia kusimangwa na kutukanwa vibaya kisa hawana hela.
“Tafadhali wanaume wenzangu, acheni kuoa wanawake mafukara… kwenu nyinyi wanawake, hiyo inaeleweka aje? Mbona kila wakati mnawaaibisha wanaume kisa ufukara? Nafikiri ni wakati wanaume waanze kuchumbiana na wanawake wenye haiba zao kupitia hali zao za kifedha,” Rudeboy alisema.