Utawala wa Kijeshi wa Kapteni Ibrahim Traoré, ambaye aliingia Madarakani Septemba 2022 kupitia Mapinduzi ya Kijeshi, atarefusha kipindi chake cha uongozi wa nchi kwa miaka mitano zaidi, kulingana na katiba iliyopitishwa Jumamosi na washiriki katika mikutano ya Kitaifa huko Ouagadougou.
“Muda wa mpito umewekwa kuwa miezi 60 kutoka Julai 2, 2024,” alisema Kanali Moussa Diallo, Rais wa Kamati ya maandalizi ya mikutano .
Rais Traoré pia ataweza kusimama katika chaguzi za Urais Ubunge na Manispaa ambao utaandaliwa ili kukomesha mpito”, aliendelea kusema Kanali Diallo.
Mikutano hiyo ya kitaifa, iliyopangwa kumalizika Jumapili, ilileta pamoja wawakilishi wa mashirika ya kiraia, vikosi vya ulinzi na usalama na hata manaibu kutoka bunge la mpito siku ya Jumamosi. Vyama vingi vya kisiasa vilisusia hafla hiyo.
Utawala wa mpito ulipaswa kumalizika Julai 1, 2024, lakini mara kadhaa Kapteni Traoré alizungumzia ugumu wa kufanya uchaguzi kutokana na mazingira ya usalama nchini.