Klabu ya Azam FC imethibitisha kukamilisha usajili wa Mshambuliaji kutoka nchini Colombia Jhonier Blanco, ambaye rasmi ataanza kuonekana kikosini msimu ujao wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara na Michuano ya Kimataifa.
Azam FC imeanza mapema usajili wa wachgezaji wake Kimataifa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kuelekea msimu ujao 2024/25, ambao unatabiriwa kuwa na ushindani mkubwa zaidi.
Kupitia Kurasa za Mitandao ya Kijamii za Klabu hiyo yenye maskani yake makuu jijjini Dar es salaam, Azam FC imeandika: GoalMachine Jhonier Blanco, ni mshambuliaji wa viwango, alikuwa mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza nchini Colombia (Categoría Primera) akiwa na Fortaleza CEIF, akifunga mabao 13, msimu uliopita 2022/23.
Blanco, alifanikiwa kuisaidia Fortaleza kupanda daraja na kuchukua ubingwa, huku akihitimisha msimu huo kwa rekodi nzuri baada ya kufunga jumla ya mabao 18 kwenye mechi 26 za mashindano yote.