Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) imebainisha kuwa WANAUME wenye umri wa miaka 50-54 ndiyo kundi linaloongoza kwa ushamiri wa Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini.
Kwa upande wa wanawake, takwimu za TACAIDS zinaonesha kinamama wenye umri kuanzia miaka 45-49 wanaongoza kwa ushamiri wa VVU huku wasichana wenye umri wa kuanzia miaka 15-24 ndiyo kundi hatarishi zaidi kwa maambukizo mapya ya VVU kitaifa.
Dk. Jerome Kamwela, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, aliyasema hayo juzi mjini Morogoro katika wasilisho lake wakati wa semina kwa ajili ya wahariri na waandishi wa habari juu ya hali ya maambukizi ya VVU, unyanyapaa, Sheria ya Ukimwi na njia bora ya kutumia vyombo vya habari kutoa elimu sahihi ya kujikinga na VVU kwa vijana.
Akirejea utafiti wa Ukimwi (THIS 2022/23), Dk. Kamwela alisema Tanzania ina watu 1,548,000 wanaoishi na VVU (WAVIU).
Mkurugenzi huyo alisema kiwango cha maambukizi mpya kwa watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 15 kimepungua kwa asilimia 16.7 kutoka 72,000 (THIS 2016/17) hadi 60,000 (THIS 2022/23).
Hata hivyo, Dk. Kamwela alisema maambukizi mapya ya VVU yameongezeka maradufu katika kipindi tajwa kwa wasichana wenye umri wa miaka 15-24.
“Utafiti unaonesha maambukizi mapya yamepungua kwa wanaume wa rika zote (watoto na watu wazima) sawa na ilivyo kwa kundi la wanawake watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 15,” alisema Dk. Kamwela na kuongeza:
“Ushamiri wa VVU kwa watu wazima (15+) ni wa asilimia 4.5, uko juu zaidi kwa wanawake (asilimia 5.6) kulinganishwa na wanaume (asilimia tatu).”
Dk. Kamwela alisema wastani wa ushamiri wa VVU ni wastani wa asilimia 1.7 mkoani Kigoma (kiwango cha chini) hadi asilimia 12.7 mkoani Njombe (kiwango cha juu zaidi).
Alitaja mikoa mitatu ya Njombe, Iringa na Mbeya kuwa juu ya wastani wa kitaifa wa ushamiri wa VVU wa asilimia tisa.