Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amefiwa na Mkwewe Marian Robinson aliyefariki jana Ijumaa asubuhi.
Marian ni mama mzazi wa Mke wa Obama, Michelle Obama na mama huyo amefariki dunia akiwa na Miaka 86.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa na familia yake imesema kuwa Robinson alifariki Ijumaa asubuhi na enzi za uhai wake alikuwa akionekana sana katika Ikulu ya Marekani katika miaka minane ya utawala wa Rais Obama (2009 hadi 2017).
Muda mwingi marehemu Marian alikuwa akiwalea wajukuu zake wawili Malia na Sasha – binti zake Michelle na Barack Obama.
Katika taarifa kwenye Mtandao wa X uliofahamika kama twitter zamani, Michelle Obama alimueleza mama yake kuwa kama mtu muhimu kwake – “jiwe la msingi ambaye siku zote alinisaidia kwa chochote nilichokihitaji”.
” Alikuwa kiungo muhimu kwa familia yetu yote na tumesikitika kutangaza kuwa amefariki dunia leo,” aliandika.
Katika ujumbe tofuati kwenye mtandao huo wa X,Bwana Obama amesema kuwa “ Alikuwepo na atasalia kuwepo Marian Robinson mmoja pekee”.
“Katika huzuni yetu tunapata nguvu kwa zawadi ya maisha yake,” aliongeza. “Na kwa maisha yetu yote tutajaribu kuishi kwa mfano wake.”
Hakuna maelezo zaidi yaliotolewa kuhusu chanzo cha kifo chake.