Kauli yake inafuatia baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kutangaza kuwa Israel imependekeza mpango wa hatua tatu kwa Hamas unaolenga kufikia usitishaji vita ya kudumu.
Mwanasiasa mkuu wa Hamas ameliambia shirika la BBC kuwa “itakubali makubaliano haya” ikiwa Israel itafanya hivyo.
Mazungumzo hayo yanakuja huku mapigano yakiendelea huko Rafah, kukiwa na ripoti za mashambulizi ya anga ya Israel siku ya Jumamosi katika mji huo ulio kwenye mpaka wa Misri na Gaza.
Hakuna hakikisho kwamba shinikizo la umma la Bw Biden kwa Israel na Hamas kuukubali mpango huo litachochea makubaliano.
Katika taarifa yake siku ya Jumamosi, ofisi ya Bw Netanyahu ilisema kuwa “masharti ya Israel ya kumaliza vita hayajabadilika”.
Amesema “kuharibiwa kwa uwezo wa kijeshi na kiutawala wa Hamas, kuachiliwa kwa mateka wote na kuhakikisha kuwa Gaza haileti tishio tena kwa Israel”.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa Israel “itaendelea kusisitiza masharti haya yatimizwe” kabla ya kukubaliana na usitishaji wa kudumu wa mapigano, na kusisitiza kwamba hakuna makubaliano yanayoweza kusainiwa kabla ya kufikiwa kwa hayo kwanza.
Siku ya Ijumaa, Bw Biden alielezea mpango huo kama pendekezo la kina la Israel ambalo lilifungua njia ya usitishaji wa kudumu wa mapigano.
Awamu ya kwanza itajumuisha usitishaji vita kamili, kuondolewa kwa vikosi vya Israel kutoka maeneo yenye watu wengi na kubadilishana baadhi ya mateka kwa wafungwa wa Kipalestina.