Kijana Innocent Chengula (23) amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam baada ya kutiwa hatiani kwa makosa sita ikiwemo kujipatia kwa njia ya udanganyifu shilingi milioni nne (4) kutoka kwa Ridhiwani Kikwete ambaye ni Mbunge wa Chalinze pia Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti na Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Siku ya tukio Mshtakiwa huyo July 26 mwaka 2022 alijitambulisha kuwa yeye ni Katibu Mkuu Dr. Hassan Abbas na kwamba Mama yake ni mgonjwa sana hivyo anahitaji msaada wa fedha kwa ajili ya kugharamia matibabu yake ambapo kwa uungwana wake bila kusita, Naibu Waziri Ridhiwani Kikwete alimtumia pesa hiyo shilingi milioni nne.
Mbali na adhabu hiyo, pia Mahakama ya Kisutu imeitaifisha simu moja ya mkononi pamoja na laini tatu za simu alizokuwa akitumia Mshtakiwa huyo na kuwa mali ya Serikali ambapo uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga na kuamuru pia Mshtakiwa huyo arudishe milioni nne za Naibu Waziri huyo.
Chengula ambaye ni Mkazi wa Kigogo Luhanga Jijini Dar es salaam, alikuwa anakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutuma ujumbe wa maandishi kwenda katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp ambapo alijitambulisha kwa Ridhiwani Kikwete na Rais wa TFF Wallace Karia kuwa yeye ni Dr. Hassan Abbas (Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii).
Related Content