Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda ametoa muda wa miezi miwili kwa Vyombo husika chini ya R.T.O kuhakikisha kila gari la TAXI linalofanya kazi katika Mkoa wa Arusha linakuwa na rangi maalum tofauti na ilivyo sasa ambapo amesema TAXI zina rangi tofautitofauti zinazopoteza mandhari na uzuri wa utalii.
Makonda ameyasema haya leo June 8 2024 kwenye Viwanja vya Magereza, Kisongo kwenye maonesho ya kimataifa ya Utalii ya Karibu Kili Fair 2024, yanayojumuisha Makampuni zaidi ya 700 ya kimataifa kutoka kwenye mataifa zaidi ya 50.
“Magari yetu ya TAXI yana rangi tofautitofauti na yanapoteza mandhari na uzuri wa utalii tuliokuwa nao, nimeelekeza Vyombo husika chini ya R.T.O vikao vinavyoendelea ndani ya miezi miwili kila gari la TAXI linalofanya kazi ndani ya Mkoa wa Arusha liwe na rangi maalum inayoonesha mandhari na uzuri wa utalii au vivutio tulivyonavyo katika Mkoa wetu wa Arusha”
“Lengo ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kutengeneza mazingira bora zaidi ya kuthibitisha ndoto ya Dr. Samia Suluhu Hassan ya kwamba Taifa na Mkoa tupo tayari kuwapokea Wageni katika Mkoa wetu, tunataka Mgeni akiingia ajue chombo anachokipanda, ajue anapokwenda na usalama wake ukiwa umezingatiwa ili azidi kurudi na kurudi tena” ——— RC Makonda.
Aidha ,katika hatua nyingine
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda amemuagiza Mkuu wa Polisi wa Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kutokukamata magari ya Utalii kwenye Mkoa wa Arusha na badala yake ukaguzi kwa Watalii ufanyike kwenye mipaka na kwenye viwanja vya ndege vinavyotumika na Watalii.
Makonda ameyasema haya mbele ya Waandishi wa habari June 08, 2024 kwenye Viwanja vya Magereza Kisongo kwenye maonesho ya kimataifa ya Utalii ya Karibu Kili Fair 2024, yanayojumuisha Makampuni zaidi ya 700 ya kimataifa kutoka kwenye mataifa zaidi ya 50.
“Kama Serikali ya Mkoa tumeona tuweke mazingira bora zaidi ya kuhakikisha kwamba Mtalii anapokuja kwenye mkoa wetu hapati changamoto na ajisikie kuheshimika kwa sababu Taifa limejiandaa kupokea Watalii, kuanzia tarehe moja mwezi wa saba tumekubaliana kwamba hakuna Polisi kusimamisha gari la Utalii”
“Hakuna kusimamisha gari lililobeba Watalii kutoka Airport au Namanga kuingia katikakati ya Mji wa Arusha, tunafanya hivyo tukifahamu ya kwamba Watalii hawa wanakuwa wamekaguliwa katika Airport au mipaka, hawana sababu yoyote ya kuwekewa vikwazo viwili vitatu vinne mpaka saba wanasimama barabarani na kupoteza muda wao” ——— RC Makonda.