HABARI KUU
Ndege ya kijeshi iliyokuwa imembeba Makamu wa Rais wa Malawi na watu wengine tisa imepotea siku ya leo Jumatatu 10 Juni 2024 na msako unaendelea, ofisi ya Rais wa Malawi imesema.
Ndege iliyombeba Makamu wa Rais wa Malawi “Saulos Chilima” mwenye umri wa miaka 51 iliondoka katika mji mkuu wa Malawi “Lilongwe”, lakini ilishindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzuzu takriban kilomita 370 (maili 230) kuelekea kaskazini, takriban dakika 45 baadaye.
Mamlaka ya usafiri wa anga ilipoteza mawasiliano na ndege hiyo hivyo mpaka sasa haijulikani ipo wapi.
Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ameamuru operesheni ya utafutaji wa ndege hiyo na ameghairi safari ya kwenda Bahamas. Juhudi zote za kuwasiliana na ndege hiyo tangu ilipopoteza mawasiliano hazijafanikiwa mpaka sasa.
Rais Chakwera ameamuru mamlaka za zinazohusika ziendeshe operesheni ya haraka ya utafutaji na uokoaji ili kujua mahali ilipo ndege.