Zimepita wiki mbili tangu aliyekuwa Rais wa Iran “Ibrahim Raisi” afariki kwa ajali ya ndege Uzi, Eastern Azerbaijan, Iran. Hapo jana tukio kama la Ibrahim Raisi limejirudia barani Afrika, kila aliyesikia habari ya kupotea kwa ndege ya kijeshi iliyombeba Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Chilima nafsi yake ilijawa na simanzi kwa sababu ni mara chache sana ndege kupotea kisha watu waliomo wakabaki hai.
Leo asubuhi taifa la Malawi limetangaza kuwa Makamu wa Rais pamoja Raia wengine 9 waliokuwa katika safari ya kutoka Lilongwe mpaka Mzuzu wamefariki kwenye ajali hiyo Chikangawa (Hifadhi ya misitu). Makamu wa Rais na Wenzake walikuwa wakielekea kwenye mazishi ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Malawi (2004-2006) na Waziri wa Katiba na Sheria (2012-2013) Raphael Kasambara aliyefariki tarehe 7 Juni 2024.
Hayati “Saulos Chilima” na Mke wake “Mary Chilima” walipendana sana kwani walipenda kusafiri pamoja katika shughuli za kikazi na binafsi. Saulos Chilima alimuunga mkono Mary Chilima kwenye taasisi zake za kusaidia watoto wenye uhitaji maalum.
Mbali na utaalamu wa Masoko, Ujasiriamali “Mary Chilima” ni Msanii pia, alishiriki kutunga na kuimba nyimbo za kumpigia kampeni Mume wake “Saulos Chilima” katika Chaguzi Mbalimbali. Wanandoa hao wamefanikiwa kupata watoto wawili “Sean” na “Elizabeth”.
Mbali hapo awali Saulos Chilima kuwa Waziri wa Wizara kadhaa aliingia rasmi kwenye siasa za ushindani akiwa mgombea mwenza wa “Peter Mutharika” katika uchaguzi wa Urais wa 2014, ambapo walishinda na akachaguliwa kama Makamu wa Rais.
Saulos Chilima alikuwa Kiongozi Shupavu, mwenye misimamo yenye tija pia alisifika kwa kupambana na rushwa.