Katika kipindi cha takribani miezi mitatu mfululizo dunia imeshuhudia wimbi la ajali za anga zilizoondoa uhai wa viongozi mbalimbali na watu walioandamana nao na kuacha hasara kubwa, mapengo katika nafasi za uongozi na vilio.
Ajali hizo ni pamoja na ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Kenya, Francis Ogolla iliyojiri Aprili mwaka huu; ajali iliyomkuta Rais wa Iran, Ebrahim Raisi iliyotokea Mei mwaka huu na hivi majuzi ajali iliyoondoa maisha ya Makamu wa Rais wa Malawi, Saulos Chilima.
Ripoti zinaonesha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Jenerali Ogolla, alifariki katika ajali ya helikopta aliyokuwa akisafiria pamoja na maofisa wengine ilipoanguka katika eneo la Kaben, Marakwet Mashariki.
Kisha mwezi uliofuata wa Mei Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Hossein Amir-Abdollahian na watu wengine saba, walithibitishwa kufariki dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea Kaskazini-Magharibi mwa Iran.
Ndipo juzi pia ulimwengu ukashuhudia ajali nyingine ya angani baada ya ndege iliyokuwa imembeba Chilima na watu wengine tisa kupotea. Ndege hiyo aina ya Dornier 228-202K ya Jeshi la Malawi ilitoweka kwenye rada za angani ilipokuwa ikijaribu kutua katika Kiwanja cha Ndege cha Mzuzu kutokana na mazingira magumu ya hali ya hewa.
Mabaki ya ndege hiyo yalipatikana baadaye katika hifadhi ya msitu wa Chikangawa, Juni 10, mwaka huu.
Bila shaka Dunia ikiwemo Tanzania ina kitu cha kuzingatia kutokana na ajali hizi na hasa mazingira ya hali mbaya ya hewa yanapotajwa.