Ni safari ya mwisho ya mtoto Noela Asimwe Novath iliyohitimishwa leo Juni 18 katika Kijiji cha Bulamura Kata Kamachumu ambapo baada ya kutekwa kutoka mikononi mwa mama yake Mei 30, Mwaka huu na jana kukutwa amefariki huku mwili wake ukiwa hauna baadhi ya viungo.
Mazishi ya mtoto huyo yamefanyika bila ya uwepo wa baba yake ambaye yupo mikononi mwa polisi akihusishwa na kutekwa kwa mtoto Asimwe pamoja na watu wengine watatu.
Akitoa salamu za serikali kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa, Mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima ameitaka jamii kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuweza kufanikisha kuwakamata wale wote waliohusika na tukio hili.
Sima Ameongeza kuwa jamii inatakiwa kuongeza ulinzi baina yao kwa kuwa serikali haiwezi kutoa ulinzi kwa kila mtu hivyo wao wanatakiwa kuwa walinzi wa wenzao.