HABARI KUU
Rais Cyril Ramaphosa leo ameapishwa kwa ajili ya mhula wa pili wa urais wa kuongoza taifa la Afrika Kusini, licha ya chama chake cha African National Congress (ANC) kushindwa kupata wabunge wengi katika uchaguzi wa mwezi uliopita.
Wabunge walimchagua tena kuwa rais wiki iliyopita kufuatia makubaliano kati ya ANC na cha upinzani cha muda mrefu cha Democratic Alliance (DA) pamoja na vyama vingine na hivyo kuunda serikali ya mseto.
Chama cha ANC, ambacho kimetawala tangu kumalizika kwa ubaguzi wa rangi mwaka 1994, kilipoteza wingi wa viti vya ubunge kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 30 na hivyo kutotoa mshindi wa moja kwa moja.
Viongozi kutoka mataifa mbalimbali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania wamehudhuria hafla hiyo.
“Ninaapa kwamba nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Afrika Kusini. Nitatii, nitazingatia katiba na sheria nyingine zote za jamhuri,” ameapa Ramaphosa mbele ya Jaji Mkuu Raymond Zondo.
Chama cha uMkhonto weSizwe (MK) kilichoundwa miezi sita iliyopita na Rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma kimesusa kikisema hakiwezi kushiriki katika uapisho huo wa “kifahari”.
Chama hicho ambacho kilipata asilimia 15 ya kura na viti 58 vya ubunge, pia kilisusia kikao cha kwanza cha Bunge Ijumaa iliyopita.