HABARI KUU
Takriban watu 34 wamekufa baada ya kunywa pombe haramu ya kienyeji inayoaminika kuwa na sumu katika jimbo la Tamil Nadu, kusini mwa India, maofisa wamesema.
Tukio hilo lilitokea katika Wilaya ya Kallakuruchi ambapo watu waliofakamia pombe hiyo walijikuta wako hoi muda mfupi baada ya kuinywa
Takriban watu 80 wako hospitalini kutokana na kunywa pombe hiyo wakisumbuliwa na matatizo ya kuhara kupita kiasi na maofisa wamesema idadi ya vifo inaweza kuongezeka.
Watu wawili wamekamatwa hadi sasa na uchunguzi zaidi unaendelea.
Mamlaka pia imemsimamisha kazi ofisa mkuu wa polisi wa eneo hilo pamoja na askari wengine 10 kwa kushindwa kuzuia uzalishaji na usafirishaji wa pombe haramu katika jimbo hilo.
Mamia ya watu hufa kila mwaka nchini India kutokana na kunywa pombe za kienyeji zinazozalishwa vichochoroni.