Siti Binti Saad (1880 – 1950), alikuwa ni mwimbaji maarufu kutoka visiwani Zanzibar. Ni miongoni mwa wanawake waimbaji wa mwanzo hapa barani Afrika.
Kwenye huu ukanda wa Afrika Mashariki, Siti Binti Saad ni mwanamke wa kipekee kwa wakati wake aliyependekezwa na kampuni ya burudani kuotka Marekani, Kolombia, kuzishughulikia santuri zilizonaswa sauti ya Malkia huyo wa Taarabu Afrika Mashariki.
Ikumbukwe kuwa Siti Binti Saad, alizaliwa katika mazingira magumu, kuwa mfinyazi vyungu mpaka alipokuja kuwa mwimbaji mashuhuri wa kimataifa.
Hakujaliwa uzuri wa kisura wala kimaumbile, bali Mola alimjalia sauti moja ya kipekee iliyowajaza wengi upendo na furaha ya kipekee.
Mola hawezi kukunyima vyote, utakosa hiki ila kile utakuwa nacho bila shaka yeyote ile.
Siti Binti Saad ni johari sii tu kwenye muziki wa Taarabu bali hata mfano moja mzuri wa kuigwa kwa wasanii wote na watu wote wasio wasanii, “tabia njema ina kishindo na sauti kubwa mno inyotawanyika kama moto nyikani.”
Siti Binti Saad licha ya umaarufu wake wakati wa uhai wake, alikuwa mtu mnyenyekevu, mwungwana, Mchamungu na mtu mwenye tabia njema. Umaarufu wake haukumfanya kuwa na dharau, kiburi au jeuri kwa mtu wa aina yeyote ile.
Hata mtunzi wa vitabu mashuhuri, Shabban Robert, alipokutana na Johari huyo wa muziki kutoka Zanzibar kwenye miaka karibia na 1950, hakuamini kuwa alikutana na Sinti Binti Saad.mwenyewe kulingana alivyokuwa mtu wa kutojikweza, na Shabban Robert akaandika kitabu mahususi, kiitwaacho, “WASIFU WA SITI BINTI SAAD”, kwa ajili ya gwiji huyo wa miondoko ya Taarabu Afrika Mashariki.
Siti Binti Saad ataendelea kukubukwa vizazi hadi vizazi.
Maisha ya Johari huyo wa Taarabu kutoka visiwani Zanzibar ni mfano hai wa methali ya Kiswahili: “Penye nia pana njia.”