Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limemchagua Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi, Wolfgang Pisa kuwa Rais wake baada ya uongozi uliopita kumaliza muda wake wa kikatiba.
Aidha, TEC imemchagua Askofu wa Jimbo la Mpanda, Eusebius Nzigilwa kuwa Makamu wa Rais.
Askofu Wolfgang Pisa alipata elimu yake Maua Seminary akasoma pia UDSM, Zambia na Marekani. Kisha kuliongoza Shirika la Wafransisko Wakupuchini Tanzania. Pia aliwahi kufundisha chuo cha SAUT tawi la Arusha.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limemchaga Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi Mhashamu Wolfgang Pisa, OFMCap kuwa Rais mpya wa Baraza hilo, huku Mhashamu Eusebius Nzigilwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda akichaguliwa kuwa makamu wa Rais wa Baraza hilo.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Juni 21, 2024 Baraza hilo pia limemchagua Padri Dakta Charles Kitima kuwa Katibu Mkuu wa Baraza hilo huku Padri Chesco Msaga akiwa Naibu Katibu Mkuu.
Taarifa hiyo imetolewa mapema leo Juni 22, 2024 na Rais aliyemaliza muda wake Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, katika Adhimisho la Misa Takatifu ya shukrani kwa Mungu kwa kupata uongozi mpya, iliyoadhimishwa katika Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili, Makao Makuu ya TEC, Kurasini Dar Es Salaam.
Askofu Mkuu Nyaisonga kwenye homilia yake amempongeza Rais mpya Mhashamu Pisa na safu yake kwa kuaminiwa na Baraza hilo huku akiwashukuru pia watendaji wote wa Sekretarieti, ambapo ametumia pia fursa hiyo kuomba radhi pale palipotokea kasoro katika uongozi wake.
Kwa upande wake Rais mpya Askofu Pisa amemshukuru Mungu na Maaskofu kwa kumpa jukumu hilo yeye na wenzake na kuongeza kuwa wapo tayari kutekeleza, ambapo amekazia kwamba kiongozi wao mkuu ni Yesu Kristo na wao ni watumishi, ambao kwa njia ya Sala na maombezi ya Kanisa wanaamini yote yatawezekana.
Aidha amempongeza na kumshukuru Askofu Mkuu Nyaisonga na Makamu wake Askofu Flavian Kassala wa Jimbo Katoliki Geita kwa kazi kubwa waliyoifanya, ambapo ameahidi kuendeleza pale walipoishia huku akiomba ushirikiano na mwongozo kila watakapobisha hodi.
Wengine waliochaguliwa kuingia katika Kamati Kuu {Permanent Council} ni Wenyeviti wa Kurugenzi mbalimbali akiwemo Askofu Mkuu Isaack Amani{Uchungaji}, Askofu Anthony Lagwen{Fedha}, Askofu Augustino Shao ALCP/OSS{Ukaguzi}, Askofu Henry Mchamungu {Sheria}, Askofu Eusebius Nzigilwa{Mawasiliano} na Viogozi wengine waliochaguliwa wataendelea kutangazwa baadaye.
Viongozi wote wapya wameapishwa leo Juni 22, 2024 katika Adhimisho la Misa Takatifu na Mwanasheria wa Baraza hilo Padri Daniel Dulle.