HABARI KUU
Rais wa Kenya William Ruto leo June 23,2024 amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na maelfu ya Vijana waliofanya maandamano ya amani wiki hii kote Nchini Kenya kupinga mapendekezo ya nyongeza ya kodi huku akiwapongeza Vijana hao kwa kujitokeza na kushughulika na mambo ya Taifa lao.
Maandamano hayo yaliandaliwa kwenye mitandao ya kijamii kisha yakahamia kwenye barabara mbalimbali za Kenya huku Washiriki wakubwa wakiwa ni Vijana Wakenya wengi wenye umri mdogo maarufu kama ‘Gen-Z’ ambao wamekuwa wakipeperusha maandamano hayo moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii.
Vijana hao wameendelea kushinikiza kutoridhika kwao kuhusu sera za kiuchumi za Serikali ya Rais Ruto ambapo Rais Ruto katika tamko lake la kwanza hadharani tangu kuanza kwa maandamano hayo akiwa kwenye Ibada kwenye Kanisa moja katika Mji wa Nyahururu katika eneo la Bonde la Ufa , amesema “Ninajivunia sana Vijana wetu, wamepiga hatua mbele kwa kufanya maandamano ya amani na ninataka kuwaambiakwamba tutawashirikisha”
Ruto amesema Serikali yake itafanya mazungumzo na Vijana hao ili kwa pamoja walijenge Taifa la Kenya liwe kubwa zaidi.