Kuelekea Uchaguzi wa Urais Nchini Marekani unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu Rais wa Nchi hiyo, Joe Biden na mpinzani wake Donald Trump wamekabiliana katika mdahalo wa dakika 90 ambao umegusa hisia za wengi nchini humo, ukiwa ni mjadala wa kwanza wa televisheni wa kampeni za uchaguzi huo.
Wawili hao wamejibizana kuhusu rekodi zao za masuala ya kiuchumi, utoaji mimba na uhamiaji katika mdahalo huo ambao kila mgombea alitafuta kumpiku mwenzake katika kinyang’anyiro kikali cha Ikulu ya White House.
Biden (81) na Trump (78) hawakusalimiana kwa kupeana mikono wakati waliposimama jukwaani katika Studio za Makao makuu ya Televisheni ya CNN mjini Atlanta.
Hakukuwa na watazamaji ukumbini na vipaza sauti vilizimwa wakati kila mmoja akizungumza. Biden ambaye aliripotiwa kuwa na mafua, alimshambulia Trump akitaka kuwakumbusha mamilioni ya watazamaji wa televisheni kuwa kama Trump atachaguliwa, atakuwa rais wa kwanza aliyehukumiwa kwa uhalifu kuingia White House.
Trump alimshambulia Biden akitilia shaka afya yake na uwezo wake wa kutamka maneno kwa sababu kuna wakati hakuwa akisikika vizuri au kukamilisha sentensi. Hata hivyo Trump amesema atakubali matokeo ya uchaguzi kama anafikiri yatakuwa ya haki.