Shahidi wa pili katika kesi ya ukahaba inayowakabili washtakiwa watano katika mahakama ya Hakimu mkazi Sokoine Drive, ameieleza mahakama hiyo kuwa waliwakamata washtakiwa hao kwa tuhuma za ukahaba kutokana na viashiria vya aina ya mavazi waliyokuwa wameyavaa na muda na waliokutwa na polisi.
Hata hivyo, Shahidi huyo ambaye ni askari kutoka Kituo cha Polisi Mburahati, WP Konstebo wa Polisi (PC), Tunusuru Malingula alijikuta katika wakati mgumu alipotakiwa kueleza maana ya ‘Umalaya’ au ‘Ukahaba’ kutokana na viashiria hivyo alivyotaja.
Ilikuwa ni wakati wa maswali ya dodoso aliyoulizwa na mawakili wa utetezi katika kesi hiyo, Peter Madeleka, Jebra Kambole na Maria Mushi, leo alhamisi Juni 27,2024 na akajibu kuwa hajui maana ya ukahaba.
Pia, amesema hajui kama kuna sheria inayobainisha sifa za mavazi yanayoashiria ukahaba wala inayoweka muda ambao mtu akikutwa barabarani anakuwa anajihusisha na ukahaba.
Shahidi huyo pia alitakiwa kueleza kama washtakiwa walikuwa miili yao, wao walibaki na nini na wateja walionunua wako wapi.
Washtakiwa katika kesi hiyi inayosikilizwa na Hakimu Mfawidhi Rachel Kasebele ni Mariam Yusuph (25) mkazi wa magomeni, Mwazani Nassoro (25) mkazi wa kigogo, Mwanaidi Salum (25) Mkazi wa Mabibo, Faudhia Hassan (35) mkazi wa Ubungo na Tatu Omary (40) Mkazi wa Ubungo.