HABARI KUU
Watuhumiwa wa mauaji ya mtoto mwenye Ualbino
Asimwe Novath aliyekuwa na umri wa miaka miwili na nusu yaliyotokea mkoani Kagera, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba leo Juni 28, 2024.
Mtoto Asimwe alitekwa na watu wasiofahamika Mei 30, 2024 nyumbani kwao katika Kijiji cha Mulamula Wilaya ya Muleba Mkoa wa Kagera na mwili wake ulipatikana Juni 17, 2024 ukiwa umenyofolewa baadhi ya viungo.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba ,Elipokea Wilson washtakiwa hao akiwemo mshtakiwa namba moja Padre wa Parokia ya Bugandika, Elpidius Rwegoshora ,mshtakiwa namba mbili ambaye ni baba wa Asimwe, Novath Venant pamoja na washtakiwa wengine saba wamesomewa shtaka la mauaji ya kukusudia.
Mkuu wa Mashtaka wa Mkoa wa Kagera ,Waziri Magumbo amesema uchunguzi wa shauri hilo umekamilika.
Hata hivyo washtakiwa hao tisa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria wa kusikiliza shauri hilo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 12, 2024 huku washtakiwa wote wakirudishwa rumande.