Rais wa Kenya William Ruto anadai kuwa hana damu mikononi mwake kufuatia mauaji ya watu yaliyoshuhudiwa wakati wa maandamano hivi karibuni.
Ruto akizungumza wakati wa kikao na wanahabari Ikulu Jumapili, Juni 30, amesema maafisa wa polisi walitekeleza majukumu yao kwa njia huru wakati wa maandamano hayo.
Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC) katika rekodi, imesema watu 23 walifariki kwa kupigwa risasi na polisi kote nchini. Zaidi ya hayo, kulikuwa na zaidi ya watu 50 waliokamatwa, 22 kutekwa nyara, na zaidi ya 300 kujeruhiwa.
Rais Ruto hata hivyo alishikilia kuwa ni watu 19 ndio waliofariki.
Kuhusu hashtag inayovuma ya ‘Ruto lazima aende’, Ruto amesema kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake.
Matamshi ya Ruto yanakuja kutokana na maandamano ya nchi nzima kupinga nyongeza ya ushuru iliyopendekezwa katika Mswada wa Fedha wa 2024.
Rais alisema kwamba kutupilia mbali Mswada wa Fedha kunamaanisha kuwa serikali haitaweza kuwaajiri walimu 46,000 wa Shule za Sekondari za JSS kwa kandarasi za kudumu na za pensheni.
Alisema kuwa bila fedha ambazo utawala wake ulitarajia kupata, haitawezekana kuwasaidia wakulima wa Kenya katika kuhakikisha wanapokea angalau Ksh.50 kwa lita moja ya maziwa.
Rais Ruto alitangaza Jumatano iliyopita kwamba hatatia saini Mswada tata wa Fedha kuwa sheria, kufuatia siku kadhaa za machafuko na maandamano katika zaidi ya kaunti 15.
Mswada huo ulikusudiwa kukusanya shilingi bilioni 346 za Kenya (dola bilioni 2.68), au 3% ya Pato la Taifa, katika mapato ya ziada.
Kenya ilikubali mkopo wa miaka minne na IMF mnamo 2021, na kutia saini kwa mkopo wa ziada kusaidia hatua za mabadiliko ya hali ya hewa mnamo Mei 2023, na kufanya jumla ya mkopo wake wa IMF kufikia $3.6 bilioni.