Gayton McKenzie, mwanasiasa wa upinzani ambaye safari yake ya maisha imezungukwa na matukio kadha wa kadha kuanzia kuwa jambazi sugu hadi mmiliki wa klabu ya burudani yenye utata, sasa ameteuliwa kuwa waziri wa michezo, sanaa na utamaduni wa Afrika Kusini.
Rais Cyril Rampahosa alimteua McKenzie, kiongozi wa Muungano wa Patriotic (PA) kushiks wadhifa huo katika serikali ya vyama vingi ambayo aliitangaza Jumapili iliyopita baada ya chama chake cha African National Congress (ANC) kupoteza wingi wake wa wabunge katika uchaguzi wa Mei 29.
Mtumiaji huyo mahiri wa mtandao wa X, (zamani Twitter), mwenye umri wa miaka 50, alifurahia uteuzi wake, akituma picha yake akiwa amevaa viatu vya soka na kuandika: “Asanteni kwa umbe wenu wa heri, nitajibu hivi karibuni. Niko mbioni kujiandaa, nina kazi ya kufanya 🥅 ⚽️.”
Kwa wandani wa McKenzie, uteuzi wake ni ujumbe kwa jamii kuonesha jinsi alivyoshinda dhiki na ibilisi ili kupata mafanikio yanayokubalija. Alishiriki kubomoa benki kwa mara ya kwanza kabla ya kufikisha umri wa miaka 16, kisha akawa jambazi kamili. Alisema hayo alipokuwa akihojiwa na kituo cha redio. Alikaa gerezani kwa miaka saba, na akaapa kubadilika baada ya kumaliza kifungo.
“Ningeweza kuwa na randi 12 mfukoni mwangu lakini nilikuwa na randi bilioni moja akilini mwangu. Na hilo ndilo watu hawaelewi – wanazingatia kile wanachokosa badala ya jinsi ya kupata kile wanachokosa,” alisema katika mahojiano ya mwakw 2013 na shirika la utangazaji la SABC.
Alikua mzungumzaji wa kutia motisha anayelipwa sana, akachapisha vitabu kuhusu maisha yake, ikiwa ni pamoja na A Hustler’s Bible, na kujitosa katika biashara mbalimbali – kutoka uchimbaji madini nchini Zimbabwe hadi vilabu vya burudani nchini Afrika Kusini – akiwa na Kenny Kunene, rafiki yake waliyetoka naye gerezani wakiwa wamebadilika.
McKenzie aliwahi kuwa na Klabu ya usiku ambayo ilifungwa na serikali kutokana na baadhi ya wateja kuendesha matendo yasiyo na maadili na Waziri huyo anasema hana mpango kurudi huko kwani ana miradi mingine.