Mamelodi Sundowns na Kocha Mkuu, Rhulani Mokwena wamefikia makubaliano ya kuhitimisha kibarua chake kwa miamba hiyo ya soka ya Afrika Kusini.
Sundowns imemshukuru Mokwena kwa mchango wake katika mafanikio na ushindi wa klabu wakati wa kipindi chake kama Kocha Mkuu. “Rhulani Mokwena daima atakuwa sehemu ya familia ya Mamelodi Sundowns na klabu inamtakia kila la heri katika juhudi zake za baadaye,” imeeleza taarifa ya Sundowns.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uamuzi wa Mamelodi Sundowns ulifanywa na Bodi kwa kuzingatia malengo na matarajio ya klabu na haukuathiriwa au kutegemea mapendekezo ya mtu yeyote anayehusiana na klabu.
Kocha Manqoba Mngqithi na benchi la ufundi wataendelea kuongoza na kusimamia mazoezi na maandalizi ya wachezaji kwa msimu ujao.
Mamelodi Sundowns imesema inajiandaa na mashindano yote yajayo, ikiwemo heshima iliyopata kwa kuwa moja ya vilabu vinne vya soka vinavyowakilisha Afrika katika Kombe la Dunia la FIFA la Klabu mwaka 2025.