Wananchi wa Uingereza wanaendelea kupiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kukirejesha madarakani chama kikuu cha upinzani cha Labour, na kumaliza takribani muongo mmoja na nusu wa utawala wa chama cha Conservative.
Huu ni uchaguzi wa kwanza wa kitaifa tangu Boris Johnson aliposhinda kwa kishindo kura ya mwaka 2019. Unafanyika baada ya Waziri Mkuu Rishi Sunak kuchukua hatua ya kushangaza ya kuitisha uchaguzi huo miezi sita mapema kuliko ilivyotakiwa.
Upigaji kura ulianza tangu saa moja kamili asubuhi kwa saa za Uingereza kwenye zaidi ya vituo 40,000 vya kupigia kura nchini kote.
Rishi Sunak alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza waliojitokeza kupiga kura katika jimbo lake la Richmond na Northallerton huko Yorkshire, kaskazini mwa England, akiwa ameongozana na mkewe Akshata Murty.
Baada ya miaka 14 madarakani chini ya mawaziri wakuu watano ndani ya kipindi cha miaka minane, chama cha Sunak cha Conservative kinatarajiwa kushindwa na chama cha Labour kinachoongozwa na Keir Starmer, chenye kufuata siasa za mrengo wa kushoto.
Starmer amepiga kura katika jimbo la Holborn na St. Pancras, kaskazini ya London, akiwa ameongozana na mkewe Victoria. Chama cha Sunak kimekuwa kikijitahidi kuwahakikishia wapiga kura kuhusu masuala kama vile kupanda kwa gharama ya maisha na mzozo katika Huduma ya Taifa ya Afya.
Kama chama Labour kitashinda, Uingereza itarudi kwenye mrengo wa wastani wa kushoto baada ya karibu muongo mmoja na nusu wa serikali za mrengo wa kulia za chama cha Conservative.
Related Posts 📫
Discover more from JUNIITV.ONLINE
Subscribe to get the latest posts sent to your email.