Mabingwa watetezi wa Kombe la Mataifa ya Amerika Kusini, Argentina imetinga nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuitoa Ecuador katika robo fainali kwa penalti 4-2.
Ushindi huo umeipa bingwa huyo mtetezi nafasi ya nusu fainali mashindano hayo kwa mara ya tano mfululizo licha ya nahodha Lionel Messi kukosa penalti ya kwanza.
Golikipa Emi Martinez alikumia mkombozi wa Argentina katika ushindi wakati mlinda mlango huyo alipookoa mabao mawili muhimu na kuiweka timu yake katika nafasi nzuri baada ya Messi kukosa penalti.
Hadi muda wa kawaida wa dakika 90 timu hizo zilikuwa sare ya 1-1 wakati wa mchezo huo uliofanyika uwanja wa NRG uliopo jiji la Houston, Jimbo la Texas, Marekani.
“Niliwaambia vijana kuwa sikuwa tayari kurudi nyumbani. Wao pia hawakuwa,” alisema golikipa Martinez baada ya kutajwa kuwa mchezaji bora wa Mechi.
Kufuatia kipigo hicho, Ecuador imemfuta kazi kocha mkuu Felix Sanchez.
“Tunamshukuru Felix na jopo lake la ufundi kwa kazi yao na weledi wao, na tunamtakia mafanikio katika jitihada zake zijazo,” Shirikisho la Mpira wa Miguu Ecuador (FEF) limeeleza.
Argentina itakutana na Canada au Venezuela katika nusu fainali huku ikitafuta kushinda taji la 6 la Copa America.